Tuesday, June 28, 2016

NAMNA YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA UJANA

UTAIINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI”. Isaya 58:12
Biblia katika Mithali 1:4 inasema ‘Kuwapa wajinga werevu, na kijana maarifa na hadhari. Pengine huu ni msatri wa ujumla wenye lengo la kumsaidia kijana awe mwenye tahadhari, mwangalifu, na ajifunze kufikiri kibiblia na kuchukua tahadhari kubwa kabla kabla ya kutenda, naam huku akitumia vema maarifa apatayo kuzishinda changamoto zenye kumkabili kila siku. Zifuatazo ni baadhi ya mbinu zitakazomsaidia kijana kuzikabili changamoto mbalimbali;
Kijana atafute kujua nini kusudi la Mungu kumleta duniani.
Wafilipi 2:13 inasema ‘Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema’. Tambua kwamba kabla hujazaliwa alikujua na akakuwekea kusudi lake unalopaswa kuliishi, maana umeumbwa ili uyatende mapenzi (kusudi) ya Mungu hapa duniani. Naam ufahamu wa kusudi la Mungu kwako utakusaidi kuishi kwa malengo na hivyo kukuepusha na kuifuatisha namna ya dunia hii.
Katika Warumi 12:2 imeandikwa ‘Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza na ukamilifu’. Kijana mwenye kujua wajibu wake duniani katika kulitumikia kusudi la Mungu atajizuia na kujiepusha na makundi mabaya, kuipenda dunia, atatumia vizuri fursa ya teknolojia kwa utukufu wa Mungu na kuwa na matumizi mazuri ya muda.
Kijana huyu atatumia muda na nguvu zake ipasavyo katika kufanya kazi zenye kumsaidia kujikimu kimaisha ikiwa ameajiriwa au amejiajiri, na ambaye anasoma atazingatia masomo kwa sababu anajua anakokwenda, hivyo hataruhusu mambo ya kipuuzi yaharibu ndoto yake (Waefeso 5:15-17 na Mhubiri 12:1). Hivyo ni jukumu lako kumuuliza Mungu ili upate kujua kwa nini upo duniani. Hata hivyo, wokovu, ufahamu wa kutosha wa neno la Mungu, kuomba kimaswali na vipawa ulivyopewa ni funguo muhimu za kukusaidia kuelewa kusudi la Mungu kwako.
Kijana ajifunze kuishi kwa imani
Waebrania 10:38 inasema ‘Lakini mwenye haki ataishi kwa imani; Naye akisi-sita, roho yangu haina furaha naye’. Pia katika 1 Yohana 2:14 imeandikwa ‘Nimewaandikia, ninyi vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi, mmemshinda yule mwovu’. Ili aweze kuishi kwa imani ni lazima kijana adumu kuongeza ufahamu wa neno la Mungu na kulitenda. Kwa kuwa chanzo cha imani ni kusikia na kusika huja kwa neno la Kristo (Warumi 10:17).
Neno la Mungu likikaa kwa wingi litaumba imani kubwa ndani yake ambayo itamsaidia kushinda kila changamoto zinazolenga kumuondoa kwenye imani husika. Maarifa yatokanayo na neno la Kristo yatamjengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na kuzikabili changamoto za ujana. Naam kuishi kwa imani kutamsiaida kijana kudumu kuwa mwaminifu na kudumu kumpenda Mungu bila kuifuatisha namna ya dunia hii na tamaa zake (Mitahli 12:1a, 1 Timotheo 4:13 – 16, Ayubu 22:19 na Waefeso 5:6).
Kijana ajifunze kuenenda kwa roho
Kuenenda kwa roho ni wito wa Mungu kwa vijana leo ili waweze kuzishinda changamoto za ujanani. Biblia katika wagalatia 5:16 inasema ‘Basi nasema enendeni kwa roho, wala hamtatimiza kamwe tamaa za mwili’. Kuenenda kwa roho ni kumpa nafasi Roho Mtakatifu ya kuongoza maisha yako sawasawa na mapenzi ya Mungu kwako.
Katika kuenenda kwa roho, siku zote, kijana anapaswa kutafakari mambo yoyote yaliyo ya kweli, ya haki, safi, yenye kupendeza, yenye sifa njema na yenye kupendeza      (Rejea Wafilipi 4:8 na Warumi 8:5). Ukweli ni kwamba kijana hawezi kuzikwepa kabisa changamoto za mwili kwa sababu mwili ni sehemu ya maisha na siku zote mwili hutamani ukipingana na roho (Yohana 3:6 na Wagalatia 5:16). Hivyo ni lazima kijana ajifunze kuenenda kwa roho ili asizitimize tamaa za mwili. 
Kijana ajifunze kuruhusu mapenzi ya Mungu yatime kuhusu mwenzi wa maisha.
Najua vijana wengi sana wamejiwekea vigezo vya wenza ambao wangependa waje kuishi nao kama wanandoa. Ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya vigezo vyao ni vya kimwili na ni kinyume na mapenzi ya Mungu kwenye maisha yao. Fahamu kwamba licha ya wewe kuwa na vigezo vya mtu unayefikiri anafaa kuwa mwenza wako na Mungu naye naye ana vigezo vya mtu anayejua anayekufaa. Naam suala la nani atakuwa mwenza wako kwa Mungu ni kipaumbele muhimu sana na ndiyo maana unapaswa kumshirikisha kwa asilimia zote ili akuongoze kufanya maamuzi sahihi (Mithali 19:14, Isaya 55:8, Mithali 16:1 na Yeremia 29:11).
Ni muhimu kijana awe makini kuhusu maamuzi anayofanya katika kitafuta mwenzi wa maisha ili yasije kuharibu kusudi la Mungu juu yake. Kijana anapaswa kujiepusha na makosa mbalimbali katika kutafuta mwenza ikiwa ni pamoja na; Kutokumshirikisha Mungu katika kutafuta mwenzi wa maisha, kufanya maamuzi ya mwenzi wake atakuwa nani ndipo aanze kuomba, Kuficha dhambi, kuwa na vigezo binafsi visivyo sahihi, na kufanya maamuzi kabla ya wakati.
Naam kuhusu vijana walioko kwenye ndoa, ni muhimu vijana hao wakajua kwamba ndoa ni wito wa mapungufu na kwamba hakuna isiyo na mapungufu, hivyo katika ndoa suala muhimu ni kila mmoja kusimama vema kwenye nafasi yake na kuchukuliana katika mapungufu yenu huku mkilenga kutafuta na kutenda makusudi ya Mungu ya kuwaunganisha.
Changamoto ni sehemu ya maisha kwa vijana, na madam tupo katika dunia hii, hakuna namna kijana atishi bila kuzikabili changamoto husika, naam jambo muhimu kijana ni kuwa makini na maisha yake akijua nafasi yake katika ufalme wa Mungu ili adumu kuyatenda mapenzi ya Mungu katika siku zake. Ni imani yangu kwamba somo hili limekuongezea maarifa katika kuzikabili na kuzishinda changamoto mbalimbali za ujanani.
Mungu wangu na akubariki na kukusaidia maana ndiye aliyeniambia ‘…utaiinua misingi ya vizazi vingi…’ (Isaya 58:12)
Utukufu na heshima vina wewe Yesu! Wastahili BWANA.
wazazi wake. Baada ya kuzungumza na huyu baba kwa upana nilikubali na kisha nikapanga muda wa kuonana na mke wake. Tulipoonana alinieleza kile kilichomuumiza na kumpelekea kuondoka kwa mumewe. Katika kuzungumza kuna wakati yule mama alisema ‘natamani huyu mwanaume angekufa kabisa’.
Binafsi nilifikiri amekosea nikamuuliza umesemaje? Akarudia tena kusema natamani afe naamini nitapata amani zaidi kwa maisha yangu yaliyosalia. Nilipomuuliza kwa nini unafikiri afe? akajibu yeye si mtu sahihi aliyepaswa kunioa, kwani walikuja wengi sana, kunichumbia, sijui kwa nini nilimkubali huyu na ndio maana leo naumia hivi.
Nami nikamwoji je unajua athari ya hayo unayosema? Hujui kwamba akifa nje ya muda na mapenzi ya Mungu, damu yake itadaiwa mikononi mwako?  Kuwaza hivyo ni kukosea sana, tayari mlishafunga ndoa, na sasa unapaswa kufikiri namna ya kubadilisha maisha ya ndoa yako kuwa kwenye hali bora zaidi na si kuendelea kubomoa. Ndipo nikamwambia ‘kama hutazijua na kuzitumia nafasi ulizopewa na Mungu, kamwe amani haiwezi kuja kwenye ndoa yako’. Ilichukua miezi yule mama kuelewa na kurejea kwenye nafasi zake, lakini ashukuriwe Mungu naye alifanyia kazi na sasa amerudi kwa mumewe wanaendelea vema.
Sikia mwanamke unayesoma ujumbe huu, madaam ulikubali kuolewa, usimpe ibilisi nafasi kwa kuwaza mabaya juu ya mume wako, ukihoji, kwa nini nilikubali kuolewa na huyu baba, au kusema najuta kuolewa na huyu baba, au laiti wangekuwa wanabadilisha wanaume ningebadilisha haraka wa kwangu nk. Kumbuka kutengemaa kwa ndoa yako ni kufanikiwa kwa makusudi ya ufalme wa Mungu hapa duniani. Changamoto mnazozipitia kama wanandoa lengo lake ni kuwatoa kwenye nafasi yenu ya kufanya kile chenye kuujenga ufalme wa Mungu.
Hivyo haijalishi mume wako kakosea nini, wewe mtwike Mungu fadhaa zako zote, na uwe tayari kusamehe na kusahau, wala usiawaze mabaya juu yake, kwa kuwa kadri unavyowaza mabaya ndivyo unavyoiingiza ndoa yako kwenye uharibifu, ndivyo unavyoyaumba na kuyaita mabaya zaidi yaje kwenye ndoa.
Nafasi yako ni ya thamani sana kwa mumeo
Katika kusoma kwangu Biblia na kufuatilia sana kuhusu nafasi ambazo Mungu amempa mwanamke, nimegundua kwamba nafasi ya mke kwa mume ni ya muhimu sana. Pengine kwa kiasi fulani inafanana na nafasi ya Kristo kwa kanisa, maana ikiwa katika ulimwengu wa roho mwanamke amepewa kuwa Msaidizi, Mshauri, Mlinzi, Mjenzi na Mleta kibali, je haya si sehemu tu ya majukumu ambayo Yesu anayo kwa kanisa lake kwa ujumla?
Nafasi ulizopewa na Mungu katika ulimwengu wa roho, ni ishara kwamba kufanikiwa kwa kusudi la Mungu kupitia ndoa yenu kunategemea sana namna ambavyo mwanamke anazitumia nafasi zake. Naam zaidi kukubalika, kustawi na kufanikiwa kila mume wako atendalo kunategemea pia namna ambavyo wewe (mke) utazitumia nafasi zako. Hivyo kuchelea kwako kutumia vizuri nafasi zako ni kukwamisha kusudi la Mungu kwenye ndoa yako, familia yako, jamii yako na taifa lako.
Ukweli ni kwamba ‘Mume wako anakuhitaji sana hata kama maneno na matendo yake hayaonyeshi kwamba anakuhitaji”. Naam, mumeo anakuhitaji kuliko unavyofikiri, kadri wewe unavyokaa kwenye nafasi yako ndivyo unavyosaidia familia yako, kijiji chako, kanisa lako na taifa lako. Naam mume wako anahitaji sana upendo wako,kumbuka upendo ndio uliomsukuma Kristo aje afe kwa ajili yetu (Yohana 3:16), ingawa hata leo wapo watu wasiomwamini, wenye kumtukana lakini yeye bado anawapenda.  Upendo wa Kristo ndani yako ukukumbushe kusimama kwenye nafasi zako kwa ajili ya mumeo.
Naam bado ningeweza kuandika mambo mengine mengi zaidi, lakini fahamu jambo hili,  laiti mwanamke akisimama na kuzitumia nafasi zake vema, mabadiliko na uponyaji mkubwa kwenye ndoa yake ni matokeo halisi ya kutarajia. Nafasi hizi tano zinampa fursa mwanamke ya kuruhusu mawazo ya Mungu kupitia ndoa yake kutimia na kuzuia mawazo ya Ibilisi kupitia ndoa yake yasitimie. Naam nafasi ya mwanamke katika ndoa ndiyo inayoamua uzima au mauti ya ndoa yake, nafasi ndizo zinazoamua kufanikiwa au kufeli kwa ndoa yake.
Hivyo endapo utayaweka mafundisho haya kuanzia sehemu ya kwanza kwenye matendo si tu ndoa yako itaponywa, bali, maombi yenu yatasikilizwa, mume wako atapata kibali mbele za BWANA, naam atakuwa mume bora katika jamii na kufanikiwa katika kila atendalo. Mahusiano na mawasiliano mazuri yatakuwa sehemu ya maisha yenu na hivyo kurahisisha kutekelezwa kwa kusudi la Mungu. Ninapomalizia ujumbe huu muhimu nakushauri usijitazame kama mwanamke wa kawaida bali jifunze kujitazama kutoka kwenye nafasi zako kama Msaidizi, Mshauri, Mlinzi, Mjenzi na Mleta kibali, naam na maisha ya ndoa yako yatabadilika.
Mungu wangu akubariki na kuiponya kabisa ndoa yako, kupitia damu na jina la Yesu, amen.

Utukufu na heshima vina wewe Yesu! Wastahili BWANA wangu

No comments:

Post a Comment