Thursday, June 30, 2016

JE, UNAFAHAMU KWAMBA UTAKATIFU NI NINI?

Je, utakatifu ni nini? Jibu ni kwamba utakatifu ni kazi ambayo Mungu anafanya ndani ya moyo wa mwanadamu ili yule mwanadamu awe mtu wa kiroho na si mtu wa dhambi. Hii ni kazi ya Mungu kumfanya mtu hai na wa kiroho, ili huyu mtu sasa hajali mambo ya dunia,bali anajali sana mambo ya mbinguni.
1. Utakatifu unajengwa juu ya neno la Mungu. Utakatifu wa ukweli si hisia ndani ya moyo, bali ni njia ya ukweli (Zaburi 119:30). Utakatifu unatoka kwa Mungu, hautoki kwa moyo wa mwanadamu.

2. Utakatifu unapatikana ndani ya moyo wa mwanadamu (Warumi 2:29). Kuna wale ambao kwa nje wanaonekana kuwa watakatifu, lakini kwa ukweli mioyo yao ni mioyo ya dhambi. Lakini yule ambaye ni mtakatifu ana na maisha ya Mungu ndani mwake. Yeye haishi maisha ya utakatifu kuwaonyesha tu watu, bali ana na utakatifu ndani mwake.

3. Utakatifu ni kazi ya Mungu, si kazi ya mwanadamu. Wakati tunazaliwa hapa ulimwenguni, tunazaliwa wenye dhambi. Biblia inatuambia kwamba dhambi inafanya kazi ndani yetu tangu tuzaliwe (Warumi 7:5), lakini utakatifu unatoka kwa Mungu (Yanabo 3:17). Yule ambaye hajaokoka hana utakatifu ndani mwake, utakatifu ni mwangaza ndani ya moyo wa mwanadamu, ni kitu ambacho Mungu anapanda ndani mwetu, ni tunda la Roho Mtakatifu (Wagalatia 5:22). Bila kazi hii ya Mungu hakuna yeyote ambaye anaweza kuwa mtakatifu.

4. Utakatifu unapatikana katika kila sehemu ya mwanadamu. Paulo aliandika, “Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, awatakase ninyi kabisa” (1 Wathesalonike 5:23). Mtu ambaye ni mtakatifu anafahamu vitu vya Mungu na anavipenda vitu hivi kwa moyo wake. Yeye ana tamaa ya kuvifuata vitu hivi na anaishi yale maisha ambayo yanampendeza Mungu. Yeye sasa ni mtu mpya (Wanalosai 3:10). Si kwamba yeye ni mtakatifu hapa na pale tu, bali ni mtakatifu katika kila sehemu.

5. Utakatifu unaonekana maishani. Hii ni kazi ya Mungu ambayo inaonekana katika maisha ya mwanadamu. Yeye haongei tu kuhusu utakatifu, bali anaishi maisha matakatifu.

6. Utakatifu ni jambo nzuri. Utakatifu ni kama dhahabu: inaonekana kuwa kitu kizuri. Yule ambaye ana na utakatifu wa ukweli hapa ulimwenguni ni kama malaika hapa ulimwenguni: yeye anaonyesha utukufu wa Mungu.

7. Utakatifu ni jambo la milele. Mungu anapanda utakatifu ndani ya moyo wa mwanadamu na hii inambadilisha yule mtu, na yeye anaanza kuwa mtakatifu jinsi Mungu alivyo mtakatifu. Wakati mtu anaokoka, hatapoteza wokovu wake: mti wa utakatifu umepandwa ndani yake na mti huu hauwezi kung’olewa.

Wafilipi 1:3-11
Katika kifungu hiki mtume Paulo anatufundisha mambo matatu muhimu: anatufundisha kuhusu ushirika wa wakristo, hakikisho la wakristo na pia maombi yake kwa sababu ya kanisa la Filipi.
Katika mstari wa 3-4 Paulo anamshukuru Mungu kwa sababu ya ushirika aliokuwa nao na kanisa hili la Filipi. Yeye anasema kwamba kanisa hili lilikuwa likishirikiana naye katika kueneza injili. Katika sehemu hii ya kifungu hiki tutaona ni ushirika wa namna gani uliokuwa kati ya Paulo na kanisa la Filipi na ulikuwa unahusu nini haswa.
1. Ushirika huu ulihusu upendo wa wandugu.
Paulo anasema, “Ninyi mko moyoni mwangu” (mstari wa 7), na katika mstari wa 8, anaongeza kusema, “Mungu ni shahidi yangu, jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote kwa huruma ya Yesu Kristo.” Mistari hii inatuonyesha ushirikiano uliokuwa kati ya Paulo na kanisa hili. Hapa tunaona kwamba mtume Paulo aliwakumbuka wapendwa hawa katika moyo wake kila wakati. Yeye hakuwakumbuka tu wakati alisikia ripoti ya jinsi kanisa hili linavyoendelea, bali alikuwa anawakumbuka kila siku. Wao walikuwa sehemu yake na pia walikuwa ndani ya moyo wake. Upendo wa mtume Paulo kwa kanisa la Filipi unatuonyesha jinsi upendo wa kweli wa wakristo unapaswa kuwa. Hii inamaanisha kwamba ikiwa hakuna upendo miongoni mwa wakristo, ni vigumu sana kuwa na ushirika. Kumpenda mtu kunamaanisha kumfanyia mtu huyo yale mambo ambayo ni mema na kushiriki naye katika mambo mema. Kumpenda mtu ni kumfanyia yale mambo ambayo ni ya faida kwake kwanza kabla ya kushughulikia mahitaji yetu. Huu ndiyo unaitwa upendo wa kujitolea, yaani upendo ambao unakufanya ufikirie kuhusu ndugu yana mkristo kwanza kabla ya kuanza kujali mambo ambayo yanakuhusu. Katika injili ya Yohana, Bwana Yesu Kristo anatuonyesha mfano wa upendo huu. Bwana Yesu anasema, “Hakuna upendo ulio mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yohana 15:13). Huu ndiyo upendo ambao kila mkristo anapaswa kuwa nao kwa wakristo wenzake. Kila mshirika wa kanisa anapswa kuwajali mandugu wenzake na kushughulikia mahitaji yao.
2. Ushirika huu ulihusu kuombeana.
Mtume Paulo anasema hapa kwamba alikuwa anawakumbuka wakristo hawa wa kanisa la Filipi na alikuwa akiwaombea. Wakati wakristo wanapoombeana, hii ni dhihirisho ya kwamba wao wana ushirika. Ikiwa tunasema kwamba tuna ushirika na wakristo wenzetu, basi tunapaswa kuombeana. Pia ni vizuri sana kanisa fulani kuyaombea makanisa mengine ambayo wanashirikiana pamoja katika kazi ya kueneza injili.
3. Ushirika huu ulihusu kusaidiana.
Paulo anasema kwamba anaomba kwa furaha sana kwa sababu ya ushirika wake na kanisa la Filipi katika kazi ya kueneza injili. Zaidi ya kuombeana, kanisa la Filipi lilimtumia Paulo zawadi. Hii intuonyesha kwamba tunaposhiriki pamoja na wakristo wenzetu hata katika kutumia pamoja mali na vitu vya dunia ambavyo Mungu ametubariki navyo, tunahimizana sana katika Bwana.
Katika mstari wa 6 Paulo anaeleza kuhusu hakikisho la wokovu wetu. Anasema, “Nina hakika kwamba, Yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataindeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu.” Hapa tunasoma kwamba, yule ambaye ameokoka amehakikishiwa maisha ya milele mbinguni. Mtume Paulo anawaeleza wakristo wa kanisa hili la Filipi kwamba anajua hawatakata tamaa kuhusu imani yao hata ikiwa watapata taabu. Hii ni kwa sababu ni Mungu mwenyewe ambaye ameanzisha hii kazi ya wokvu ndani mwao. Hivi ndivyo anawaambia Wafilipi, “Yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu ataiendeleza na kuikamilisha.” Maneno ya Paulo hapa yanatukumbusha kwamba wokovu ni kazi ya Mungu mwenyewe. Mtu hapati wokovu kwa sababu amefanya uamuzi wa kumkubali Yesu Kristo. Wokovu wa mtu hautengemei bidii yake kamwe ama matendo yake. Ni Mungu mwenyewe ambaye anamwonyesha mtu dhambi zake kwa kufanya kazi yake ndani ya moyo wa mtu. Katika kitabu cha Waefeso 1:4, Biblia inasema, “Mungu alituchagua katika Yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake.” Hii inatuonyesha wazi kwamba kabla ya Mungu kuumba ulimwengu alipanga mpango wake wa kuwaokoa wenye dhambi. Hii ndiyo sababu Paulo anawaeleza wakristo wa Filipi kwamba wanapaswa kuwa na hakikisho kwamba baada ya maisha ya hapa ulimwenguni wao watakuwa na Kristo milele mbinguni. Tunapaswa kujua kwamba Mungu hatazuiliwa na chochote, chochote ambacho alipanga kitatimika.
Tena Paulo anawaeleza Wafilipi kwamba Mungu ataikamilisha kazi ambayo ameanza ndani mwao. Wokovu ni kazi kuu ya Mungu. Katika kazi hii Mungu anampatia uzima mtu ambaye alikuwa amekufa katika dhambi na manasa. Pia Mungu anamwonyesha huyu mtu uovu wa dhambi zake. Halafu, Mungu anampatia mtu toba na imani ndani ya Yesu Kristo na anamhesabia haki. Baada ya kufanya haya yote, Mungu anaanzisha kazi ya kumtakasa mtu ili afanane na Kristo mwenyewe. Hii kazi ya kumtakasa mtu ili afanane na Kristo Yesu ni kazi ya maisha yote wakati mtu ana hapa ulimwenguni. Mungu mwenyewe ataendelea kufanya kazi hii katika mioyo ya wale ambao wameokoka hadi siku ile watatoka humu duniani. Mungu ataendelea kufanya kazi hii katika mioyo ya watu wake hadi siku ile wataingia mbinguni.
Maombi ya Paulo kwa Wafilipi (mistari 9-11).
Kuna mambo mawili ambayo Mtume Paulo anaomba kwa ajili ya kanisa la Filipi katika hii barua yake.
(i) Upendo. Paulo anasema, “Haya ndiyo maombi yangu kwamba upendo wenu uongezeke zaidi katika maarifa na ufahamu wote.” Kanisa la Filipi lilikuwa kanisa ambalo washirika wake walipendana sana, kwa hivyo Paulo anawaeleza waendelee kuwa na huu upendo wa mandugu zaidi na zaidi. Paulo anawaombea kwamba upendo wao kwa mandugu wenzao uwe ni wa kujua zaidi neno la Mungu ili washirika wote waweze kujua ni mambo gani yaliyo mazuri ya kufanyiana katika kila hali.
(ii) Maisha matakatifu. Katika mistari ya 10-11 Paulo anasema, “Ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ile ya Kristo, mkiwa mmejawa na matunda ya haki yapatikanayo kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa za Mungu.” Ishara ya mkristo wa kweli ni maisha matakatifu. Biblia inasema kwamba Mungu “Alituchagua katika Yeye kabla ya kuumbwa ulimwengu ili tuwe watakatifu na bila lawama mbele zake” (Waefeso 1:4). Yesu mwenyewe alisema, “Ni heri walio na moyo safi, kwa maana hao watamwona Mungu” (Mathayo 5:8). Pia tunasoma katika kitabu cha Waebrania kwamba bila kuwa na utakatifu hakuna mtu atakayemwona Mungu (Waebrania 12:14). Ikiwa mtu anasema kwamba ameokoka lakini anaishi maisha ya dhambi, basi ukristo wake si wa kweli. Yeye hajaokoka kwa sababu ishara kubwa ya wokovu, yaani kuishi maisha matakatifu haionekani ndani mwake.

No comments:

Post a Comment