Mara
nyingi wapendwa tunaposoma habari ya laana tunaichukulia kama jambo jepesi na
kuona kuwa laana hizi ni kama hazipo ama hazitupati na ndio maana watu
tunaendelea kucheza na mambo ya Mungu. Lakini leo nataka kukuonyesha kuwa laana
hizi zipo na zinaonekana wazi wazi katika maisha yetu. Mambo mengine
yanaonekana kama ya kawaida katika maisha yetu lakini kimsingi mambo hayo
hayatakiwi kuwapata watu wa Mungu. Hebu sasa tuangalie baadhi ya laana ambazo
Mungu amesema. Nabii Hagai anaanza kwa kusema, ”Basi sasa Bwana wa majeshi
asema hivi, zitafakarini njia zenu“ (Hagai 1:5)
Maana
mambo haya yanatokea kwenu; soma mstari wa 6.
Mnakula lakini hamshibi, mnakunywa lakini hamjazwi na
vinywaji. Hii ni hali ya kutotosheka na chakula maana unakuta mtu anakunywa na kula
lakini baada ya masaa kadhaa anakula na kunywa tena.
Jambo
hili linaharibu bajeti yake kwa kujikuta ametumia hela nyingi kwenye chakula
bila sababu ya maana. Bwana anao uweza wa kuondoa hiyo nguvu ya tamaa ya kula
na kunywakunywa ovyo na kukufanya utosheke na chakula kidogo na cha kawaida.
Mnajivika lakini hampati joto. Hii
ni tamaa ya mavazi. Mtu anajikuta hataki nguo au mtindo wa mavazi umpite japo
hata kama uwezo wa kufanya hivyo hana. Sisemi kwamba kuvaa ni vibaya lakini
lazima tuwe na kiasi na hasa wakati ambapo kipato chetu hakijafikia hatua ya
kwenda na fashion.Watu wengi bajeti zetu zimeathiriwa na tamaa ya mavazi.
Yeye apataye mshahara anaweka katika mifuko iliyotoboka
toboka. Hii ndio mbaya kuliko zote maana
kuna wakati mtu unafanya kazi na kupata mapato yako lakini baada ya siku mbili
tatu pesa yote imekwisha na wala ulichofanya cha maana hakionekani na wakati
mwingine ni rahisi kuona kuwa labda mtu amekuibia.
Mlitazamia vingi vikatoka vichache, tena mlipovileta
nyumbani vikapeperushwa. Kuna
wakati mwingi tunafanya kazi na pengine ngumu sana tukitazamia kupata kipato
kikubwa lakini matokeo yake yanakuwa madogo. Pengine tunafanya biashara lakini
faida inatoka kidogo sana. Pengine tunafanya kazi kwa bidii lakini mabosi wetu
ndio kwanza wanatudharau.
Mbingu zimezuiliwa zisitoe umande Na nchi isitoe matunda. Hii inatokea pale ambapo nguvu ya Bwana ya mbaraka
inapokuwa haipo juu yako. Hivyo hata kama utafanya biashara yaani utapanda
mbegu (Mtaji) hutafanikiwa.
Kumbukumbu la Torati 28:15 – 68
- Mstari wa 21 – 22: Bwana atakuambatanisha na tauni
- Mstari wa 23: Mbingu zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma
- Mstari wa 24: Bwana atafanya mvua ya nchi yako kuwa mavumbi na mchanga
- Mstari wa 28: Bwana atakupiga kwa:
- Wazimu
- Upofu
- Bumbuwazi la moyo
- Utakwenda kwa kupapasa papasa
- Hutafanikiwa katika njia zako
- Utaonewa na kutekwa nyara
Mstari wa 32: Wanao na binti zako watapewa taifa jingine - Na macho yako yataangalia na kuzimia kwa kutamani mchana kutwa
- Hapatakuwa na kitu katika uwezo wako
- Mstari wa 33 Matunda ya nchi yako na taabu yako yote vitaliwa na taifa usilolijua
- Mstari wa 37 – 40 Wewe utakuwa
ushangao, na mithali, na dharau kati ya mataifa, mbegu nyingi utapanda
shambani lakini utavuna haba kwa kuwa nzige watazila.
- Mstari wa 43 Mgeni aliye katika nchi yako atazidi kupaa na wewe kushuka
- Mstari wa 44 Yeye atakuwa kichwa na wewe mkia
- Mstari wa 48
- Mstari wa 49 - 51 Bwana atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai, taifa usilolifahamu ulimi wake, taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala halipendelei kijana. Naye atakula uzao wa ngombe zako uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa, wala hatakuachia nafaka ,wala divai, wala mafuta, wala maongeo ya ngombe wako, wala mwana kondoo wako mpaka utakapokwisha kuangamizwa
Yeremia
5:1– 9
Hebu
sasa tuangalie maisha ya wapendwa wengi makanisani mwetu. Watu wengi ndani ya
makanisa ya watu tuliookoka tumetembea chini ya laana hizi kwani ni kweli
kwamba wapendwa wengi maisha yetu kwa ujumla wetu ni duni sana. Laana ambayo
imesemwa katika Kumbukumbu la Torati 28:28 ndio hasa imetawala ndani ya watu wa
Mungu. Wengi tumepigwa na upofu hatuoni chochote cha kutuendeleza katika maisha
yetu. Wakati watu wa mataifa wanaona mambo makubwa, wanavumbua miradi mikubwa,
watu waliookoka kwa sababu ya kutokwenda sawasawa tumejikuta kuwa hatuoni
chochote kile. Kwa ujumla, wapendwa, laana hizi zipo na zinatembea ndani ya
watu wa Mungu. Yatupasa kuamua kama alivyosema Joshua: Hakuna jinsi ya kupona,
njia pekee ni kujisalimisha kwa Bwana Mungu wetu.
BARAKA
Baraka
ni nguvu ya Mungu ya uwezeshaji wa Mungu katika maisha ya mtu. Kweli sisi
tuliookoka tunaposema habari ya baraka tunakuwa tunasema habari ya Mungu
kuachilia nguvu au uwezeshaji ndani ya maisha yetu. Kumbukumbu la Torati 8:18 ”Bali
wewe utamkumbuka Bwana Mungu wako maana yeye ndiye akupaye nguvu ya
kupata utajiri.“ Katika eneo hili neno nguvu lina maana ya:
-ufahamu
-maono
-kibali
-uvumilivu
-bidii
pamoja na mambo mengine ambayo yatakufanya wewe kupanda juu kwa haraka ambayo
Mungu ameikusudia.
Kila
mtu aliyeokoka anatakiwa kuwa na nguvu hii kusudi aweze kufanikiwa katika
maisha yake. Panapokuwepo hii nguvu, maisha ya mtu aliyeokoka katika hali
yeyote lazima yatabadilika na kuwa mazuri zaidi ya yalivyokuwa mwanzo. Hivyo
kila mtu aliyeokoka yampasa kuitafuta na kuhakikisha nguvu hii ipo kwake.
MFANO WA NGUVU (BARAKA)
- Yusufu alikuwa mtoto mdogo miaka 17 tu
- Alikuwa anafanya kazi ndogondogo za nyumbani,
- Alipenda kukaa na wazazi wake
- Yusufu alimcha Bwana naye alichukia dhambi na ndio maana alipendwa na Mungu. (Mwanzo sura 39). Ndugu zake Yusufu walimchukia sana Yusufu, nao wakamuuza, naye akaenda kuwa mtumwa.
YUSUFU KAMA MTUMWA
Katika
hali ya kawaida Yusufu alikuwa kama watumwa wengine tu, lakini kwa Yusufu
ilikuwepo nguvu ya Mungu (uwezeshwaji wa Mungu). Mstari wa 2 ”Bwana akawa
pamoja na Yusufu“ Uweza wa Bwana wa kustawisha ulikuwa pamoja na Yusufu.
KAZI YA UWEZA HUU
Nguvu hii huleta ustadi wa kazi
Yusufu
alipewa ustadi wa kazi, wakati wowote Yusufu alipopewa kazi aliifanya kama
bwana wake (Potifa) alivyotaka, na hivyo kuufurahisha moyo wa bwana wake
(Potifa). Mwanzo 39:3”bwana wake akaona ya kwamba Bwana yu pamoja naye ,na ya
kuwa Bwana anafanikisha mambo yote mkononi mwake.“ Nguvu hii ni ya muhimu sana
katika maisha yetu. Nguvu hii ni ya muhimu katika biashara zetu na kazi za aina
yoyote.Tutakapoweza kufanya kazi au biashara kwa ustadi, na kwa akili ya
KIMUNGU, basi jua mafanikio ni makubwa sana.
Nguvu
hii huleta kibali.
Mwanzo
39:4. ”Yusufu akaona neema machoni pake akamtumikia“ Kibali ni jambo muhimu
sana kwetu sisi ikiwa ni kazini ama kwenye biashara, maana watu wakitupenda
ndivyo watakavyokuja kwa wingi kwenye biashara zetu, na mabosi wetu watatuwazia
mema wakati wote. Tutakapoingia sehemu yeyote na kusema neno au tendo basi
tutaonekana sisi kwanza
Nguvu hii huleta bidii
Tunaona
Yusufu alivyofanya na kumaliza kila kazi aliyokuwa amepangiwa na hivyo bosi
wake kuona ampe majukumu makubwa zaidi. Kama Yusufu angekuwa stadi na ana
kibali lakini kazi zinalala, bwana wake asingempa majukumu makubwa.
Nguvu hii huleta uvumilivu
Wote
tunafahamu maisha ya mtumwa, hutumwa hovyo, hupewa kazi nyingi, tena ngumu,
lakini Yusufu alivumilia akachapa kazi na watu wale wakashangaa. Pamoja na
mengine mengi nguvu ya Bwana ilimfanya Yusufu kuonekana si mtu wa kawaida
katika nyumba ya Potifa.
Nguvu hii huatamia yale ambayo tunayafanya,
Mstari
wa 5 ”…mbaraka wa Bwana ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba na
katika shamba.“ Kusudi uweze kufanikiwa unatakiwa kuwa na nguvu hii juu
yako.Mungu wa Yusufu ndiye Mungu wetu; kama alivyokuwa na Yusufu ndivyo
atakavyokuwa na sisi pia. Jambo la kukumbuka: palipo na mbaraka huu haijalishi
wewe ni wa namna gani. Katika sehemu zote mbili alizopitia Yusufu, ya utumwa na
ufungwa utaona mwisho wa Yusufu ni juu sana.
Hali
uliyo nayo isikufanye kukata tamaa bali tafuta mbaraka wa Bwana uwe maishani
mwako. Kutokusoma, kutokuwa na mtaji, kutokuwa na refa, sio sababu ya kukufanya
wewe kutokufanikiwa maana wewe ni mtu ambaye unawezeshwa na NGUVU maalum ya
Mungu katika maisha yako. Nguvu hii tunaiona tena katika maisha ya Yakobo
nyumbani kwa Labani, Mwanzo 30:25-43
Yakobo
hakuwa na mahari ya kukomboa wake zake na watoto wake kusudi aweze kwenda
kuishi mwenyewe, hivyo aliamua kufanya kazi nyumbani kwa mkwe wake Labani.
Lakini tunaona wazi tangu mwanzo wakati Yakobo amefika kwa Labani. Labani
hakuwa tajiri kama baada ya kukaa na Yakobo. Utajiri wa Labani
ulipatikana baada ya mtu mwenye nguvu ya Baraka ya Mungu kushika mali
zake. Mstari wa 27, ”…maana nimetambua ya kwamba Bwana amenibariki kwa ajili
yako“
Mstari
wa 30. ”Maana mali yako ilikuwa haba kabla sijaja…Bwana akakubariki kila
nilikokwenda“
Mtu
wa Mungu ambaye nguvu ya Mungu ya ongezeko imo ndani yake anapofanya
jambo lazima hilo jambo lifanikiwe sana. Baada ya Yakobo kuwa na wanyama wake
na Labani kuwa na wanyama wake, nguvu ya Baraka ya ongezeko ilikuwa
juu ya wanyama wa Yakobo, hivyo basi Yakobo aliongezeka sana mpaka ukoo wa
Labani ukaanza kumuonea wivu. Mwanzo 30:43, ”Kwahiyo mtu huyo akazidi mno akawa
na wanyama wengi na wajakazi na watumwa na ngamia na punda.“ Mungu wa Yakobo
ndiye Mungu wetu.
Yesu anapofundisha habari ya nguvu hii anasema. ”…msisumbuke
basi mkisema,
(1)Tule
nini, (2)Tunywe nini, (3)Tuvae nini?“ (Mathato 6:24-33). Mstari wa 35, Maana
watu wasio na Mungu, wasio na nguvu hii ya baraka kutoka kwa Mungu hao ndio
wanaosumbuka. Lakini sisi Baba yetu wa mbinguni anajua kuwa tunataka hayo naye
ataleta nguvu hiyo ya kutuwezesha ili kutufanya tuwe nayo yote tunayoyahitaji.
Mstari wa 33. Hivyo basi utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na hiyo
nguvu na yote yatakuja.
Mwandishi wa Zaburi anasema katika Zaburi 1:1-3:
Heri,
amebarikiwa, amepewa nguvu, atafanikiwa mtu yule, aitendaye sheria ya Bwana. Mstari
wa 3, kila alitendalo litafanikiwa.
Wapendwa
yatupasa kwanza kuitafuta hiyo nguvu ndipo tutakapoona mambo makubwa na ya
ajabu yakitendeka maishani mwetu. Wana wa Mungu yatupasa kuelewa kuwa (BARAKA)
nguvu hii ya kutuwezesha ni roho kamili toka kwa Mungu kama tunavyoona Mungu
mwenyewe anamwambia Musa katika kitabu cha Kutoka 31:3 - 4 Nimejaza Roho ya
Mungu ndani yake. Roho hii ya Mungu ambayo Mungu ameweka au anaweka ndani yetu
inaleta mambo yafuatayo
-
Hekima
-
Maarifa
-
Ujuzi wa mambo ya kazi za kila aina
Kutoka 35:31–35. Naye amejaza Roho ya Mungu katika
-
Hekima
-
Akili
-
Ujuzi
-
Kazi za ustadi
-
Kuvumbua kazi za werevu
-
Amejazwa akili za moyoni.
Roho
hii itakapokuwapo juu yako nataka kukwambia huwezi kuwa masikini lazima neno la
Mungu litimie kwako lile linalosema ”Na watu wote watakuita mbarikiwa“ Nguvu
hii au Roho hii kamili toka kwa Bwana haitolewi kwa upendeleo bali ni kwa
kila mtu aliyeokoka na kukubali kutembea katika njia za Bwana. Kumbukumbu la
Torati 28:1-2 Bwana anaweka msimamo jinsi ya kupokea nguvu hii ya muhimu kwenye
maisha yetu; anasema ”Itakuwa utakapoisikia sauti ya Bwna, Mungu wako, kwa
bidii, kutunza kufanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana Mungu
wako atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya dunia na Baraka hizi zote
zitakujilia na kukupata“
Hebu tutazame mambo yafuatayo:
1.
Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana Mungu wako
2.
Kwa bidii
3.
Kutunza kufanya maagizo yake yote
Matokeo:
Ndipo
baraka (Nguvu) hizi zote zitakujilia na kukupata Isaya 1 :19 ”Kama mkikubali na
kutii mtakula mema ya nchi.“ Warumi 2:10 ”Bali utukufu na heshima na amani kwa
kila mtu atendaye mema…“
(Mambo
ya Walawi 26:3 – 13, Kumbukumbu la Torati 8:12 – 15). Pamoja na maandiko
mengine mengi utaona ya kuwa siri kubwa ya kupata mbaraka au nguvu hii ni
kutenda sheria ya Bwana. Hapo juu tumeona mambo matatu muhimu ambayo
Mungu anataka kwetu.
- Kusikia sauti ya Bwana, kinyume sana na tulivyozoea watu wengi tunapokuwa na pilika ya kutafuta pesa tuna kosa muda wa kuja kanisani kwenye mafundisho na hata tukirudi nyumbani tumechoka hatuwezi kusoma Neno. Lakini kumbe kama tunataka kuendelea yatupasa kujitahidi sana kusoma Neno na kuhudhuria mafundisho. Ndani ya Neno utaona wazi wazi yale ambayo Mungu anataka tufanye na yale ambayo Mungu hataki tufanye.
- Kwa bidii, tunaona tena wazi pale ambapo tunatafuta pesa, watu wengi tunaweka bidii sana kwenye pesa , lakini sharti la Bwana linasema tulitafute Neno kwa bidii sana.
- Kutenda sawasawa, tunapaswa kutenda sawaswa na yale ambayo Mungu ametuagiza kutenda
Tutakapokuwa
tumefanya mambo hayo tutaona wazi wazi nguvu ya Bwana ya mbaraka ikiwa juu yetu
.
Maombi.
Hatuwezi
kuwa na kiu na bidii ya kusoma Neno pamoja na kutenda sawasawa kama
tutakuwa sio waombaji. Maombi ndio njia pekee ya kutupatia nguvu za kuweza
kuyatenda hayo. Kwa kifupi kabisa niseme hivi nguvu ya Mungu ndani ya maisha
yetu italetwa na mambo makuu matatu
-
Kusoma neno kwa bidii
-
Kutenda sawa sawa na neno
-
Kuomba kwa bidii
Baada
ya kuona mambo ambayo yatatupata tutakapokuwa chini ya laana ama tutakapokuwa
chini ya mbaraka wa Mungu tutazame sasa neno MTAJI.
MTAJI
Wana
wa Mungu tunapoongelea mtaji, watu wengi wanafikiri tunataka kuzungumzia pesa
na wanakuwa wapo sawa kabisa. Lakini leo nataka kukupa jambo la msingi kwetu
sisi watu wa Mungu.
Kwetu sisi watu wa Mungu mtaji wetu wa kwanza ni kuhakikisha nguvu ya Mungu ya mbaraka (baraka) ipo kwetu.
Nguvu hii inapokuwepo kwetu swala la pesa sio tatizo.
Tunajifunza
neno hili kwa Yakobo katika kitabu cha Mwanzo 29 na 30. tunaona wazi wakati
Yakobo anakwenda kuoa hakuwa na pesa ya kulipa mahari hivyo alilazimika kulipa
mahari ya nguvu zake na hivyo alitumika miaka kumi na nne ili kupata wake wote
wawili.
Katika
miaka yote kumi na nne Yakobo aligundua kuwa nguvu ya Bwana ya mbaraka ilikuwa
juu yake na ndio maana Labani alipomwambia kwamba sasa nitakulipa mshahara
aligoma. Alijua kwamba mshahara ungezuia nguvu ya Bwana ya kumuongeza na
kumkuza. Mwanzo 30:30 ”Maana mali yako ilikuwa haba kabla sijaja, nayo imezidi
kuwa nyingi. Bwana akakubariki kila nilikokweda…“ Kwa maana nyingine Yakobo
anamwambia Labani ”Nguvu ya Bwana iliyo juu yangu ndio imekuongeza kiasi hiki
ulichonacho, sasa wewe utanilipa nini cha kutosha?“
Mstari
wa 31, ”Akamwuliza, Nikulipe nini? Yakobo akasema USINIPE KITU“.
Yakobo akijua
kuwa nguvu ya mbaraka ya Bwana ipo juu yake alitaka mali kidogo toka kwa Labani
na Labani bila kufahamu hilo alikubali kwa urahisi kabisa. Soma mstari wa 32-33
.
Katika
mstari wa 43, Biblia inasema, ”Kwa hiyo mtu huyo akazidi mno, akawa na wanyama
wengi…“ Utajiri tayari.
Wapendwa,
nguvu ya Mungu ya mbaraka inapokuwapo upande wetu chochote kile
kinachotuzunguka ni mtaji tosha.
Katika
hali hii tuliyonayo yatupasa kutafuta nguvu ya Mungu ya mbaraka kwanza kabla ya
mtaji wa pesa. ”Tafuteni ufalme wa Mungu kwanza na haki yake yote mengine
yote mtazidishiwa“ Yesu anaendelea kusema ”Msisumbuke kama mataifa.“ Kwa
maneno haya sisemi tusitafute pesa, pesa tutafute lakini yatupasa kujua kuwa
pesa sio msingi wa maendeleo kwetu sisi tuliookoka. Kwetu sisi kitu cha
kwanza ni kibali cha Mungu katika maisha yetu. Ni nguvu ya Mungu katika
maisha yetu ya kila siku. Neno la Mungu linasema katika Kumbukumbu la Torati
kwamba Mungu ndiye atupaye nguvu za kupata utajiri. ”Bali utamkumbuka
Bwana Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri…“(Kumb 8:18).
Hatua ya pili ni pesa
Baada
ya nguvu ya Mungu kuwepo kwetu nasi tukaanza na chochote kidogo kilichopo, hata
kama ni kibaya, au cha fedheha, tutaona Bwana anatufanikisha, na yale mapato
yanayoingia ndio unakuwa mtaji wetu mzuri wa kuanzia.
Fedha
yoyote tunayopata yatupasa kuitenga au kuiweka katika makundi matano muhimu.
Yaani fedha kwa ajili ya:
- Zaka (Fungu la kumi)
- Sadaka (Dhabihu)
- Mtaji
- Akiba
- Chakula.
Mtaji
lazima uongezeke kila wakati tunapohesabu faida. Kwa maana hiyo basi tunapokuwa
tayari tumepata faida yatupasa kutenga kiasi cha fedha yetu na kuiweka kwenye
mtaji. Kwa mfano: Nilianza biashara bila kitu pale Kamanga Feri; nilianza
nikiwa mpiga debe tu. Samaki zinapoletwa, mimi nachukua toroli na kuanza kuuza
huku mwenye samaki hizo amekaa tu. Chochote nachopata kwa siku au kwa wiki
lazima nitenge sehemu kidogo ya mtaji. Ikiwa makubaliano yetu ni kuwa kila
samaki nitakaye muuza yeye atanipa shilingi 100 basi nikiuza samaki 50 ninapata
shilingi 5,000 kwa siku. Kwa wiki shilingi 5,000 x 6 = 30,000.. Kwa mwezi
30,000.00 x 4 = shilingi 120,000.
Kwahiyo
hizo shilingi 120,000 zinapaswa kugawanywa katika yale mambo matano muhimu
(zaka, sadaka, mtaji, akiba na chakula).
Nguvu
ya Mungu inapokuwepo, kiasi kidogo tu cha pesa chatosha kuwa mtaji wa kutuletea
mambo makubwa. Mtaji mkubwa wa pesa ni kitu cha muhimu sana lakini kisiwe
kizuizi kwetu sisi kuanza kufanya yale ambayo tunakusudia kufanya katika maisha
yetu.
Yakobo
akijua kuwa anayo nguvu ya Mungu ya mbaraka maishani mwake anamwambia Labani,
sitaki unilipe pesa ”nipe lile kundi dogo la wanyama wenye marakaraka hao ndio
utakuwa mshahara wangu.“ Labani bila kujua hilo anamkubalia Yakobo. Na Yakobo
mwenye nguvu ya Mungu anaanza na yale machache na mwisho wake tunaona Yakobo
anakuwa tajiri.
Hivyo
nakushauri wewe uliyekata tamaa na maisha, hapo ulipo na kipato ulichonacho
chatosha kukufanya wewe kuwa tajiri sana sana.
Tunapokuwa
tumeanza kupata pesa yatupasa kujua kuwa kilichotuwezesha ni nguvu ya mbaraka
maishani mwetu na sio ujanja wetu, hivyo ni lazima tuhakikishe kuwa
tunaitunza hiyo nguvu ya Mungu ya mbaraka maishani mwetu. Na ili kutunza hiyo
nguvu maishani mwetu yatupasa kufanya mambo yafuatayo.
1. KUTOA
ZAKA
(i)
Zaka ni sehemu ya kumi (10%) ya mapato yako yote, ambayo Neno linasema ni mali
ya Bwana. Mambo ya Walawi 27: 30 ”tena zaka yote ya nchi kama ni mbegu ya nchi
au kama ni matunda ya nchi ni ya Bwana, ni takatifu kwa Bwana.“
(ii) Zaka itolewe wapi?
Hesabu
18: 21 ”Na wana wa Lawi nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao
badala ya huo utumishi wautumikao, maana ni utumishi wa hema ya kukutania.“
Hesabu
18:24 ”Kwakuwa zaka ya wana wa Israeli waisongezayo kuwa zaka ya
kuinuliwa kwa Bwana n mewapa Walawi kuwa urithi wao …“
Kumbukumbu
18: 1-5. Mstari wa 1 ”makuhani Walawi kabila yote ya Lawi wasiwe na
fungu wala urithi pamoja na Israeli watakula sadaka za Bwana...“ Zaka ni
kwa ajili ya MAKUHANI WALAWI. Maana wao hawakupewa urithi (mashamba wala
ajira) bali Bwana ndiye urithi wao kwa hiyo zaka unatoa kanisani kwako
unapopata malisho ya kiroho na anakula Mchungaji wako yule anayeilea roho yako
na atumikaye mbele ya madhabahu ya Bwana kwa ajili ya roho yako.
(iii) Sababu ya kutoa zaka.
Malaki
3 : 10-12
(a)
Ufanye chakula kiwemo kwa wingi nyumbani mwa Bwana. Zaka hutolewa kwa Bwana
lakini anayekula ni Mchungaji wako, pale unapopokea malisho. Kama tulivyoona
watumishi wa Mungu hawana urithi, Bwana ndiye urithi wao, hivyo chakula
kinapokuwepo tele nyumbani mwa Bwana unamfanya Mchungaji wako kutulia na
kutafuta malisho ya kutosha kwaajili ya Kanisa. Nehemia 13: 10-12 mstari
wa 10 ”Tena nikaona ya kwamba Walawi hawakupewa sehemu zao, basi wamekimbia,
Walawi na waimbaji, waliofanya kazi kila mtu shambani kwake.“ Unapoacha
kutoa zaka unasababisha mchungaji wako badala ya kutafuta malisho kwa ajili ya
kondoo, atafute kazi ya kumpatia chakula na kwa hiyo kanisa litakosa malisho
bora na hasira ya Bwana kuwaka juu ya kanisa
(b) Zaka huonyesha ni kiasi gani mtu anamcha Bwana kwa mapato yake. Kumbukumbu 14: 22- 23, Mithali 3:9 ”Mheshimu Bwana kwa mali yako na kwa malimbuko ya mazao yako yote.“
(c) Unapotoa zaka unasababisha Bwana kufungua madirisha ya mbingu tayari kumwaga baraka tele Malaki 3:10d ”…mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka hata isiwepo nafasi ya kutosha au la ..“
(d) Unapotoa zaka pia Bwana anawafukuza maadui wafuatao: Malaki 3: 11
(i)
Alaye
(ii)
Aharibuye mazao yenu
(iii)
Apukutishaye mazao yenu kabla ya wakati
Toa zaka usifanye nyumba ya Mungu kuachwa na Walawi (makuhani) hata wasipoiacha Mungu hashindwi kuwalisha au kuwahudumia, bali laana itakuwa juu yako wewe. Kumbukumbu 28:23 ”… na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma“ Soma pia Hagai 1:4–11. Hayo ni matokeo ya kudharau nyumba ya Bwana.
2.
KUTOA SADAKA
Sadaka
ni kiasi cha mali zetu ambacho mtu anatoa kwa Mungu kwa hiari yake mwenyewe
kulingana
na vile ambavyo mwenyewe amependa au amemthamanisha Mungu wake. Paulo
ameifananisha sadaka na mbegu, inapotolewa ni sawasawa na kupanda mbegu ndani
ya shamba.
2
Wakorintho 9;1-14. Hivyo chukua moyoni mwako picha hii kwamba kutoa ni
kupanda na sadaka yako ni mbegu inayopandwa ndani ya shamba. Katika mstari wa 6
Neno la Mungu linasema, ”Apandaye haba atavuna haba, apandaye kwa ukarimu
atavuna kwa ukarimu.“ Ukarimu ni nini? Ni moyo wa kumwaga kwa wingi, pasipo
kuzuilia. Mithali 11;24-25 ”Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi, kuna
azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji. Nafsi ya mtu mkarimu
itawandishwa; Anyweshae atanyweshwa mwenyewe.“ Mithali 19:17 ”Amhurumiaye
maskini humkopesha Bwana, naye atamlipa kwa tendo lake jema“
Hivyo
sharti la kwanza tunapokwenda kupanda mbegu zetu yatupasa kujua kuwa lazima
tupande kwa wingi, mwenye kipimo kimoja apande kwa wingi katika kipimo alicho
nacho, mwenye vipimo kumi apande kwa wingi kwenye vipimo vyake kumi, mwenye
vipimo ishirini, hamsini, mia kila mmoja lazima apande kwa wingi. Kumbuka
hatupandi kwa kutazamana, bali kila mmoja anapanda kwa kadiri ya kipimo
alichonacho na katika kipimo ulicho nacho panda kwa wingi.
2
Wakorinto 9;7 ”Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa
huzuni wala si kwa lazima, maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa
ukunjufu.“
Sharti
la pili juu ya sadaka yetu, ni lazima iwe kwa moyo wa kupenda, hiyari ya moyo,
ndiyo tabia yetu kutoka ndani. Ukweli kama tunataka kufanikiwa na kuona nguvu
ya mbaraka inatukalia yatupasa kujijengea tabia hii maishani mwetu, kufurahi na
kushangilia wakati wa kutoa, maana tunajua kutoa ni kupanda mbegu.
Mambo
manne ya kutazama
(1)
Kusudi la moyo
(2)
Sio kwa huzuni
(3)
Sio kwa lazima
(4)
Kwa moyo wa ukunjufu
Mungu
anapoyaona mambo hayo ndani yamaisha yetu.
(i)
Unapanda kwa wingi
(ii)
Unalo kusudi la kupanda wakati wowote unapoona shamba
(iii)
Hupandi kwa huzuni
(iv)
Hupandi kwa lazima,
(v)
Unapanda kwa moyo wa ukunjufu.
Kwa
ujumla Bwana anapoona hayo ndiyo maisha yako kutoka ndani anafanya yafuatayo;
(a)
Anakujaza kila neema kwa wingi. Neema ni Nguvu/uweza unaomfanya mtu kuweza
kufanya jambo ambalo alikuwa hawezi kulifanya.
(b) Unakuwa na riziki za kila namna. Anamwaga Roho ya Mungu ndani yako kusudi uongezeke na kuwa na riziki za kila namna.
(c) Upate kuzidi sana katika kila tendo jema, anakuzidishia ili na wewe uzidi sana katika kutenda mema. 2 Wakorintho 9; 10 ”Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda,na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye ataongeza mazao ya haki yenu.“
Tunapopewa
kipato katika hali yoyote ile, yatupasa tujue katika kipato hicho, kuna mambo
mawili,
(i)
Kuna mbegu ya kupanda na
(ii)
Kuna mkate wa kula.
Tutakapotambua
haya basi, yatupasa kujua mambo yafuatayo yanatokea: Atawapa mbegu za kupanda
na kuzizidisha. Pili, ataongeza mazao ya haki yenu. Matokeo ya kupanda
mbegu ni Bwana kuzizidisha na kuongeza mazao yako. Katika mstari wa 11
imeandikwa, ”mkitajirishwa katika vitu vyote.“ Yaani matokeo ya kupanda mbegu
ni watu wa Mungu kutajirishwa kila upande katika vitu vyote. Sadaka, Dhabihu,
mbegu ni vitu vya muhimu sana kwa mtu uliyeokoka ambaye unataka kufanikiwa na
kuongezeka. Tunapokuwa tumetoa sadaka au dhabihu kwa moyo wa kupenda na kwa
wingi Bwana atatuongeza kwa
- kutumwagia Roho yake juu yetu.(Ujuzi na ustadi mkubwa wa kuyafanya yale tunayoenda nayo)
- Kuongeza ufahamu (Maono makubwa)
- Kibali
3.
MAOMBI
Kwa sababu
adui yetu shetani anajua kuwa hawezi kutushinda tunapokuwa na Bwana, anajaribu
kutufanya tuache kufanya mapenzi ya Mungu maishani mwetu.
Wapendwa
sio rahisi wala sio jambo la mchezo mtu kutoa fungu la kumi, ni pale tu mtu
anapokua na nguvu ya Mungu ya kumuwezesha maishani mwake ndipo mambo mengine
yanaonekana kuwa rahisi.
Sio
rahisi kutoa ili kuwasaidia wajane na yatima, na kupeleka injili, pasipo mtu
kuwa na nguvu ya Mungu maishani mwake. Na nguvu hii ya Mungu tunaipata kwenye
maombi. Pasipo maombi hatuwezi kupata nguvu ya Mungu ya kutusaidia kutenda
mema.
Kwa
kifupi unaposikia sadaka na fungu la kumi jua kuwa ni NGUVU ya Mungu katika utu
wetu wa ndani ndiyo inayotuwezesha kutenda hayo.
Pia
watu wengi wameshindwa kufanya mambo makubwa katika maisha yao kwasababu ya
kushindwa kwenye vita na roho za upinzani. Wapendwa, zipo roho za upinzani sana
katika maisha yetu hasa tunapokuwa tunakwenda kwenye mambo yatakayomletea Bwana
utukufu. Zipo roho za kukatisha tamaa, kuvunja moyo, kuzuia, zote hizi kiboko
yake ni maombi makali. Maana maombi hushusha nguvu za Mungu, huvunja mapingu,
huvunja kuta.
Hivyo
pamoja na kufanya biashara kama watu wa Mungu yatupasa kujua kuwa maombi ni ya
muhimu sana sana.
4.
KUFANYA KAZI KWA BIDII
Wapendwa
kama tulivyoona Bwana amekuwa akiwabariki wale ambao wamekuwa wakifanya kazi
kwa bidii, maana tunaona Mungu analeta nguvu ya kutuwezesha, na sio kumwaga
baraka kama mvua.
Neno
la Mungu linasema katika Zaburi 1-3 ”…Na kila atendalo litafanikiwa“ Tunapokuwa
tunafanya jambo ndipo Mungu analeta uwezeshaji katika yale ambayo tunayafanya.
Kumbukumbu la Torati 28:8 ”Na mambo yote utakayotia mkono wako“ yatafanikiwa.
Mstari wa 12 ”Na kubariki kazi ya mkono wako.“ Yatupasa kufanya kazi kwa
mikono yetu ndipo tutaona nguvu ya mbaraka inakuwa pamoja nasi na kutufanikisha
Jambo
tunalotakiwa kujua ni kuwa tunapofanya kazi yatupasa kufanya kazi kwa bidii pasipo
ulegevu wala kujionea huruma. Tunaona hata Yusufu pamoja na nguvu
ya Mungu kuwa juu yake lakini alifanya kazi kwa uwezo wake wote. Mwanzo 39
Biblia inasema Yusufu alipewa kazi zote za nyumbani na shambani na alifanya
akamaliza. Kuna maandiko mengi yanayotuonyesha kuwa mtu mwenye bidii
atafanikiwa sana. Mithali 10:4; Mithali 12:24; Mithali 13:4; 1 Wafalme 11:28;
Mithali 22:29; Mithali 6:6-11.
Wapendwa
wengi tunakosa bidii katika mambo yetu na ndio maana hatufanikiwi.
Jambo
jingine la muhimu ni kutochagua kazi. Yatupasa kuwa tayari kufanya kazi yoyote
huku tukijua kuwa ndio mwanzo wa mbaraka wetu
Katika
kitabu cha Ruthu tunaona wazi wakati Ruthu alipokuwa na shida alikwenda kufanya
kazi ya chini kabisa lakini mwisho wa Ruthu ulikuwa wa ajabu sana.
Ruthu
2:3a Neno la Mungu linaonyesha Ruthu aliamua kwenda kondeni kuokota masazo
nyuma ya wavunaji. Ruthu 2 3b Neno la Mungu linasema ”Bahati ikamfikia“Bahati
ya Ruthu haikumkuta nyumbani wala kwenye mkesha wala amefunga mlimani, bahati
ilimkuta kwenye shughuli.
Ruthu
2:5 Mwenye shamba aliyekuwa tajiri alimwona akampenda
Ruthu
2:8-18 Ruthu akapata kibali mbele ya mwenye shamba na mambo mengine mazuri
yakaendelea mpaka maisha ya Ruthu yakawa mazuri sana
Wapendwa
tusibweteke, tufanye kazi kama watu tunaoamini kwamba Mungu anatupenda na
kutuwazia mema.
5.
KUWA NA MIPANGO (MALENGO)
Watu
wengi tuliookoka huwa hatuna mipango (malengo). Mtu anafanya vitu kutokana na
msisimko au ameona mtu fulani amefanya au amefanikiwa ama amesikia ushuhuda kwa
juu juu kuhusu mtu fulani. Basi anaanza na yeye kuingia pasipo mipango au kujua
misingi na njia alizopitia mpaka kufikia hapo alipo. Mara zote unapotaka jambo
lolote kubwa au nzuri ni lazima ulipangie mipango na uiheshimu mipango ile na
kuitendea kazi kwa gharama yoyote ile. Yeremia 29:11 ”Maana nayajua
mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana…“ Mungu wetu ni Mungu wa mipango na
tunapohitaji baraka ni lazima tuwe na mipango juu ya baraka hizo. Maana hata
wokovu wetu Mungu aliupangia mipango tangu mwanadamu alipokosa pale bustanini
Edeni. Mwanzo 3: 15.
Kuna
mipango ya maendeleo ya aina mbili
- Mipango ya muda mfupi
- Mipango ya muda mrefu
Mipango
ya muda mfupi:
Hii
ni mipango ambayo wengi tunaikimbia kwa sababu haina utukufu kwa maana waweza
kujikuta unafanya kazi au shughuli za hovyo kitu ambacho wengi hatutaki. Lakini
kwa ntu aliyeokoka ambaye anajua kuwa Bwana ni nguvu zake yeye anakuwa
tayari kwa lolote.
Mipangi
hii mara nyingi ni mizuri sana kwani ina mambo yafuatayo
- Haihitaji mtaji kubwa
- Haihitaji elimu kubwa
- Haihitaji kujulikana sana
- Mara nyingi hutumika kama kianzio kwa ajili ya mambo makubwa
Mambo
muhimu ya kuzingatia wakati umo ndani ya mipango hii
- Uvumilivu mkubwa
- Lengo lako la mbele
- Kujituma sana
- Katumia gharama kidogo kadiri utakavyoweza – Kwani mara nyingi mapato yake huwa kidogo sana
- Maombi na kusoma Neno (kuhakikisha Bwana yuko pamoja na wewe)
Mipango
ya muda mrefu:
Mipangi
hii ni mizuri sana kwani huzaa mambo makubwa katika maisha yetu. Mipango hii
inataka mambo yafuatayo
- Mtaji wa kutosha
- Elimu ya kutosha juu ya shughuli unayokwenda kufanya
- Usimamizi wa kutosha
- Maombi makubwa na kusoma Neno
ASANTE KWA MAFUNDISHO MAZURI
ReplyDelete